Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Joseph Kakunda amezindua mpango wa mashindano ya mbio za baiskeli na kufanikisha kukusanya Sh. milioni 280 kati ya Sh milioni 340 zinazotarajiwa kukusanywa kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini.
 
Mashindano hayo yamepewa jina la ‘Imara Pamoja Cycle Challenge’, yameandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji wa Madini nchini -Acacia kwa kushirikiana na Tasisi binafsi kutoka nchini Canada – CanEducate.
 
Akizungumza katika uzinduzi wa uchangiaji wa mashindano hayo juzi jijini Dar es Salaam, Kakunda alitoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kujitokeza kuchangia mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 3, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
 
Kakunda ambaye alimwakilisha Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, alisema malengo ya mashindano hayo yanaenda sambamba na malengo ya serikali katika kurahisisha mazingira ya utoaji elimu nchini.
 
“Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani na kufuta ada za shule pamoja na ada za ziada, hadi mwaka jana kumekuwapo na ongezeko la asilimia 44 la uandikishaji wanafunzi wapya wa elimu ya awali, ongezeko la asilimia 33 la uandikishaji wanafunzi wapya wa darasa la kwanza na wanafunzi wapya wanaojiunga na elimu ya sekondari wameongezeka kutoka 366,396 mwaka 2015 hadi 483,216 mwaka 2017,” alisema Kakunda.
 
Aidha, ameongeza kuwa hatua hizo zinahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali kama wanavyofanya Acacia katika kufikia malengo ya serikali.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Acacia nchini, Asa Mwaipopo alisema kwa mwaka jana pekee kampuni hiyo imejenga madarasa na kukarabati mabweni yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 100 wa kike katika Shule ya Sekondari Mwendakulima iliyopo wilayani Kahama.
 
  • Breaking News: Mbunge Mwingine Chadema ajiuzulu na kuomba kuhamia CCM
  • Shonza akerwa na watafuta kiki mtandaoni, Sister Fey atajwa
  • Mbunge Neema azidi kumwaga misaada Njombe, agusa maisha ya wananchi
 
Naye Rais wa taasisi ya CanEducate, Rishi Ghuldu alisema kila mwaka taasisi hiyo huwezesha kielimu wanafunzi 270 na kutoa nafasi 11 za udhamini wa masomo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali duniani.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 9, 2018
Soko kubwa la samaki kuhamishwa