Baraza la taifa na Hifadhi ya Mzingira NEMC limepewa mwezi mmoja na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina kupima Vumbi, Moshi na Maji yanayotoka katika kiwana cha kuchakata taka cha SBS kilichopo katika maeneo ya Mangamba Mjini Mtwara ili kujirisha kama vina madhara kwa mazingira na viumbe hai.

Naibu Waziri Mpina akiwa katika muendelezo wa Ziara yake ya kukagua mazingira na kuangalia utekelezaji wa sheria ya mazingira kwa wenye viwanda nchini amelitaka baraza hilo kufanya kazi zake kwa makini na kuto kukubali majibu ya vipimo toka kwa mwekezaji bila NEMC pia kufanya vipimo na kupata majibu sahihi kutokana na sababu kuwa wananchi wamekuwa wakilalamika mara kwa mara juu ya uchafuzi wa mazingira unaofanywa na wenye viwanda unavyo hatarisha maisha yao na mazingira kwa ujumla.

Aidha Katika Ziara Hiyo ya Mjini Mtwara, Naibu Waziri Mpina Pia alitembelea DAMPO la kisasa la mjini hapo lililojengwa kwa ufadhili wa Bank ya Dunia lenye thamani ya shilingi Bilioni 8.8 na kuwapongeza wananchi wa Mtwara kwa kupata Dampo la kisasa ambalo ni Rafiki wa Mazingira, na kutoa ushauri kwa waratibu wa mradi huo na uongozi wa mkoa wa Mtwara kuanza kutumia DAMPO hilo.

Awali, akitoa taarifa ya Mazingira ya Mkoa wa Mtwara, katibu Tawala wa Mkoa huo  Alfred Luanda, alisema kuwa mkoa unakabiliana na changamoto mbalimbali za kimazingira ikiwa ni pamoja na uvuvi haramu wa kutumia mabomu, ukataji miti ovyo kwa matumizi ya kuni na mkaa, vitendea kazi pamoja na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.

Ziara Ya naibu Waziri  Mkoani Mtwara  ilihusisha pia kutembelea bandari ya mtwara ili kujionea utekelezaji wa sheria ya mazingira katika uingizwaji wa viwatilifu na kemikali hatarishi kwa mazingira zinazoingizwa  kupitia bandari hiyo.

Video: 'Top10' ya ndege kubwa zaidi Duniani
Video: Makonda amekuja na mkakati mwingine wa Dar es salaam