Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja leo Julai 21,2021 ametembelea eneo la Tendaguru Mkoani Lindi linalosifika kwa kutoa mabaki ya mjusi mkubwa Duniani anayejulikana kwa jina la Dinosaur ambaye ni kivutio kikubwa cha utalii katika jumba la Makumbusho nchini Ujerumani .
Mabaki yake yaligunduliwa miaka 100 iliyopita katika eneo hilo na yalikusanywa na kupelekwa nchini Ujerumani ambako wataalamu waliyaunda na kisha kuyaweka kwenye Makumbusho ya nchi hiyo.
Akiwa katika eneo hilo Mhe. Mary Masanja amesema Wizara yake kwa kushirikiana na wadau itahakikisha inaendelea kulitunza eneo hilo ili litumike kwa utalii utakaoongeza pato la Taifa.
Amesema Serikali ina makusudi makubwa ya kuhakikisha Dinosaur anatangaza utalii wa Tanzania ulimwenguni kote.
Ameiagiza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lindi kusimamia wafugaji wasivamie eneo la Tendaguru ili kutunza mazingira ya asili ya eneo hilo.