Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameipongeza Kampuni ya DataVision International kwa hatua nzuri zilizofikiwa za utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Sekta ya Ulinzi Binafsi nchini kwa njia ya kielektroniki (PSGP) unaoendeshwa na kampuni hiyo na Chama cha Sekta ya Ulinzi Binafsi TSIA chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi.
Masauni amesema hayo wakati akifungua rasmi mkutano mkuu wa mwaka wa Chama Cha Sekta ya Ulinzi Binafsi Tanzania (TSIA), uliofanyika katika makao makuu ya nchi Jijini Dodoma kwa kukutanisha wamiliki wa makampuni ya ulinzi wanachama wa TSIA kutoka Kanda zote za sekta ya ulinzi binafsi Nchini.
Ametoa pongezi kwa kubuni mradi huo wa kusimamia na kuratibu sekta ya ulinzi binafsi kwa kutumia TEHAMA mbao amesema ni wa kipekee na kwamba utakuwa ni suluhisho la changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya ulinzi binafsi, na wizara yake itafaidika kwa kuweza kuratibu sekta muhimu katika ulinzi wa taifa letu kwa weledi mkubwa.
Awali, katika hotuba yake ya ufunguzi, Masauni ametoa pongezi kwa makampuni binafsi ya ulinzi kwa kuongeza kufanya kazi kwa nidhamu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika shughuli zao licha ya kukumbana na changamoto mbalimbali.
Pi amezungumzia baadhi ya changamoto zilizo tajwa katika risala ya TSIA ikiwepo kukosekana kwa sheria inayoongoza sekta ya ulinzi binafsi ambayo ameeleza kuwa linafanyiwa kazi kwa haraka na kuahidi kulisimamia litekelezwe kwa haraka.
Masauni ameendelea kueleza kuwa changamoto nyingine ni pamoja na ununuzi na umiliki wa silaha, kuwa na utaratibu unaochukua muda merfu hadi kutolewa kibali jambo ambalo ameahidi kujadiliana na viongozi wa Jeshi la Polisi kupata ushauri wa kitaalamu ili kulishughulikia swila hilo.
Aidha, amesisitiza umuhimu kwa makampuni kuendeleza ushirikiano na Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yao, ushirikiano ambao amekiri kuwa utaimarika pindi sheria itakapo kamilika na kupitishwa, jambo ambalo pia litapunguza uwepo wa kampuni holela za ulinzi zinazojihusisha na uhalifu.
Masauni ametoa wito kwa makampuni ya ulinzi binafsi kuhakikisha wanajali maslahi ya wafanyazi wao, jambo ambalo litasaidia kupunguza uhalifu. Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanaajiri wafanyakazi walio na historia nzuri, pia kawataka wazingatie matumizi ya silaha na utunzaji wake kwani imebainika ziko silaha zinazo tumika kwenye uhalifu ambazo vibali vyake vilitolewa kwa makampuni binafsi ya ulinzi.
Amewataka kuhakikisha zinakaguliwa hadi idadi ya risasi zinazo toka na zinazo ingia, na kufuata kanuni na sheria za matumizi ya silaha na usalama.
Amezitaka kampuni binafsi za ulinzi kufuata sheria na haki za binadamu kwa kuhakikisha wanawapeleka wahalifu mahakamani kwani katika nchi yetu ni mahakama pekee ndiyo iliyopewa mamlaka yakutoa maamuzi na adhabu kwa wahalifu na sio kujichukulia hatua mikononi.
Mkutano huu mkuu wa mwaka wa Chama Cha Sekta ya Ulinzi Binafsi Tanzania (TSIA) umehudhuriwa na wajumbe kutoka kanda zote za nchi, nyanda za juu kusini, kanda ya kati, Arusha, Tanga, Iringa, Morogoro, kanda ya aiwa na Dar es salaam pamoja na wadhanini wa secta ya ulinzi binafsi akiwepo IGP mstaafu Said Mwema.