Polisi jijini Nairobi nchini Kenya wanamshikilia askari aliyepoteza bastola yenye risasi 15 akiwa bar katika eneo la Uhuru Camp.
Askari huyo aliripoti kupoteza silaha hiyo akidai kuwa alikuwa katika bar moja na rafiki zake, lakini alipofika nyumbani kwake aligundua kuwa hana silaha.
Taarifa ya polisi iliyoripotiwa na Standard Media ya Kenya imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo alieleza kuwa aliondoka bar baada ya kujisikia kizunguzungu na hali ya kutaka kulala ghafla.
“Ameeleza kuwa aliegesha gari lake pembeni ya barabara karibu na bar hiyo na aliposhtuka alielekea nyumbani na ndipo aligundua kuwa hana bastola yake yenye risasi 15. Bastola hiyo inaweza kuingia mikononi mwa wahalifu, hivyo tunamshikilia,” imeeleza.
Tukio hilo limekuja wakati ambapo Bodi ya Leseni za Silaha za Moto ikiweka kanuni ngumu zaidi za umiliki wa silaha hizo kwa watu binafsi.
Bodi hiyo imeeleza kuwa inaendelea kufanya ukaguzi wa silaha hizo na kwamba hadi sasa imebaini kuwa kati ya leseni 15,000 za silaha za moto, leseni 3,000 ni feki.
Wamili wote wa silaha za moto nchini humo hivi sasa wanakaguliwa na kuandikishwa kwa mfumo wa kielektroniki.