Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Dkt. Fred Matiang’i amesema kuwa vyombo vya usalama nchini humo vimedhibiti majengo ya 14 Riverside ya jijini Nairobi yaliyoshambuliwa na magaidi leo mchana.
Matiang’i ameuambia umma kuwa kutokana na oparesheni ilivyofanywa na vitengo maalum vya usalama, nchi hiyo imerejea katika hali ya usalama na hali imedhibitiwa.
“Tumedhibiti majengo yote ambayo yalikuwa yanadhibitiwa na washambuliaji. Ninaweza kutangaza sasa kuwa nchi yetu iko salama na watu wanapaswa kuendelea na majukumu yao ya kawaida,” amesema Matiang’i.
“Tunawashukuru marafiki zetu, taasisi za kimataifa kwa ushirikiano waliouonesha kwetu. Ninapenda kuwaeleza Wakenya kuwa ugaidi hautaweza kutushinda, na sisi kama nchi hatutajisalimisha au kuyumbishwa kwa namna yeyote,” ameongeza.
Amesema kuwa amemtaarifu Rais Uhuru Kenyatta kuhusu kila kinachoendelea na amewataka Wakenya kuendelea kuwa watulivu.
Picha za CCTV zilizotolewa usiku huu zinawaonesha washambuliaji watatu wakiingia kwenye jengo hilo, wakirusha risasi kadhaa nje ya jengo na kuingia ndani.
Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limekiri kuhusika na tukio hilo, likieleza kuwa limefanya oparesheni ndani ya jiji la Nairobi.
Watu kadhaa wameuawa na wengine wamejeruhiwa, ingawa bado taarifa rasmi haijatolewa kuhusu madhara ya tukio hilo.