Shuhuda wa tukio la kigaidi lililotekelezwa leo katika hoteli ya kifahari ya Dusit D2 iliyoko kwenye majengo ya 14 Riverside jijini Nairobi, ameeleza jinsi walivyowahi kuliona gari ambalo leo limebainika kuwa lilikuwa na magaidi.
Shuhuda huyo mwenye duka katika jengo hilo, aliyehojiwa na kituo cha runinga cha Ktn akijitambulisha kwa jina la James, amesema kuwa wamewahi kuliona gari hilo mara nne katika eneo hilo, na leo wameliona dakika chache tu kabla ya magaidi kushambulia eneo hilo.
“Tulikuwa tunaliona gari hili ambalo liliingia na magaidi. Tulikuwa na wasiwasi nalo kwa sababu limekuwa likija mara kadhaa. Muda ambao limekuja, watu walitoka ndani ya gari hilo wakaingia kwenye hili jengo na kuanza kufanya mashambulizi,” ameeleza James.
Alieleza kuwa walilishuku gari hilo kwakuwa mara zote lilikuwa likifika katika eneo hilo lakini halikuwa likichukua abiria kama gari ni ‘Uber’, lakini mtu mmoja tu alikuwa akishuka.
“Hatukuwa tunaona idadi ya watu kwakuwa gari ilikuwa na vioo vyeusi (tinted), lakini kwa kawaida mtu mmoja amekuwa akishuka na kuingia kwenye jengo. Gari lao ni aina ya Toyota Ractis,” aliongeza.
James has been seeing the supposed car that was being used by the attackers. He recounts the number of times he has been seeing the car #RiversideAttack pic.twitter.com/iPo1Kj2iKV
— ktn (@KTNKenya) January 15, 2019
Gari hilo linalotajwa na shuhuda huyo, linaonekana likiwa katika eneo hilo la tukio wakati huu ambapo vikosi vya usalama vya Kenya vikiendelea kufanya uokoaji na kuwadhibiti magaidi hao.
Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limekiri kutekeleza tukio hilo likidai kuwa linaendelea kufanya oparesheni yake jijini Nairobi.
Shambulizi hilo lilianza majira ya saa tisa mchana na hadi wakati huu (saa moja usiku) bado Jeshi la Polisi linaendelea kufanya oparesheni maalum katika jengo hilo.
Watu kadhaa wamejeruhiwa na wengine wamepoteza maisha, idadi kamili bado haijatolewa na jeshi la polisi. Hospitali ya Avenue pekee imepokea majeruhi 16 na hospitali ya Kenyatta imepokea majeruhi wanne na Hospitali ya Nairobi imepokea majeruhi mmoja.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Joseph Boinnet amewataka Wakenya kuendelea kuwa watulivu na kwamba jeshi la polisi linawadhibiti vilivyo magaidi hao.
Tukio la leo, limetokea tarehe sawa na ile ya mwaka 2016 (Januari 15), ambapo Al-Shabaab walivamia kambi ya el-Adde yenye Muungano wa Majeshi ya Afrika nchini Somalia ambapo ilielezwa kuwa askari 63 wa Kenya waliuawa. Jumla ya wanajeshi 180 waliripotiwa kuuawa na kundi hilo la kigaidi.