Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umeendelea kukomaa na usajili wa mchezaji atakayevaa jezi namba sita ‘06’, ambayo ilikuwa ikitumiwa na Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ aliyetimkia Azam FC.
Kwa muda wa majuma kadhaa Uongozi wa Young Africans umekuwa ukizungumza kuhusu usajili wa mchezaji huyo, ambaye inadaiwa anatokea nje ya nchi.
Afisa habari wa Young Africans Ally Shaban Kamwe amesema mipango ya usajili wa mchezaji huyo inaendelea vizuri, na mapema juma lijalo itakamilishwa na muhusika kutambulishwa kwa Mashabiki na Wanachama kupitia vyanzo vya habari vya klabu hiyo.
“Hadi kufika Jumanne (Julai 17), tutakuwa tumemaliza zoezi zima la utambulisho wa sajili zetu. Watu wanafikiri utambulisho wa Jonas Mkude ndio namba 6 tuliyoisema, bado namba sita hajatangazwa”
“Yeye atakuwa ni mtu wa mwisho kutangazwa, siku akitangazwa mfano kuwasimulia watu wengine kuhusu unyama na ukatili alionao huyu jezi namba 6 wananchi wataingia mtaani kufurahia, itakuwa ni kama sikukuu ya mwaka mpya. Tukimtambulisha mafataki yatapigwa, ngoma zitapigwa, nyimbo zitaimbwa kila pande ya nchi hii watu watafurahi”
“Tutamtambulisha kabla ya wiki ya Wananchi, Kaizer Chiefs wao watakuwa watu wa mfano kuwasimulia watu wengine kuhusu unyama na ukatili alionao huyu jezi namba 6.” Amesema Ally Kamwe
Hadi sasa Young Africans imeshatangaza usajili wa wachezaji wawili wazawa Nickson Kibabage akitokea Singida Fountain Gate na Jonas Mkude akitokea Simba SC, huku Gift Fred akiwa mchezaji pekee wa Kimataifa akitokea Uganda.