Mdau wa soka nchini Tanzania Erick David Nampesya amejitokeza hadharani na kuonesha namna alivyoguswa na tukio la kiungo mshambuliaji wa Simba SC Bernard Morrison, ambalo limechukua nafasi kubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Morrison anashambuliwa mitandaoni kufuatia tukio la kumpiga kiwiko beki wa Ruvu Shooting Juma Nyoso, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu uliomalizika kwa Simba SC kufungwa bao moja kwa sifuri.
Nampesya ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook namna alivyoguswa na tukio hilo, lakini akaonyesha kumtetea Morrison ambaye kwa siku za karibuni amekua hachezi kwa kiwango cha kuridhisha kama alipokua Young Africans.
Nampesya ameandika: Soka ni mchezo wa kiungwana sana, niwe mkweli, awali sikupenda Morrison asajiliwe Simba, lakini baada ya kuwa amesajiliwa.
Ninampenda Morrison kwa sababu Simba ni sehemu ya maisha yangu.
Kuhusu kitendo cha kumpiga ngumi Juma Nyosso, simtetei kama mchezaji kwa sababu hakupaswa kufanya alichofanya, ila kutokana na mfululizo wa Rafu na Vipigo, Mitama na Vifuti dhidi ya Morrison ambavyo amekuwa akitendewa huku Waamuzi wakipeta.
Tukio la leo (Jana) nililitarajia, kwa Sababu matendo yale hayakuwa kwa bahati mbaya hata kidogo, na hakika waliopanga kuwa wanamfanyia walijipanga kikamilifu na hatimaye wamemfikisha walipotaka na kwa sababu Morrison pia alizaliwa na mwanamke. Nilijuwa tu uvumilivu utamshinda.
Rungu litampitia sawa tu ila kitakachonisikitisha ni Morrison kutokuwa na Skills za Zlatan Ibrahimovich.
Kwa wasiofahamu Marco Materazzi aliwahi kumchezea rafu huyu jamaa nadhani wakiwa mazoezini timu moja kule Italia, kisha ikapita miaka kadhaa wakaja kukutana baadae Materazzi akimkaba Zlatan, alichofanya Zlatan alihakikisha Materazzi anaenda wodini kwa ajili ya matibabu, baada ya Kumpa Mambo ya Kikweli.
Ndiyo maana mimi ni shabiki mkubwa wa Zlatan Ibrahimovich, na nasikitika hakuwahi kuchezea Liverpool, ingekuwa inawezekana tungemuazima ili kumtuma kwa Pickford.
Pole Sana Morrison, sisi wanyama Followers tunakupenda kinoma sana, yaani kuliko juzi na jana.