Uongozi wa Klabu ya Namungo kesho Jumatano (Juni 14) unatarajia kukutana kupitia ripoti ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2022/23 na kufanya tathmini kabla ya kuanza maandalizi ya msimu ujao wa ligi.

Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Ally Selemani, amesema kuwa kamati ya utendaji itakutana kesho kuweka mikakati kwa ajili ya msimu mpya wa 2023/2024.

“Hatuwezi kuanza mipango ya msimu ujao kabla hatujapitia ripoti ya msimu huu na kuifanyia tathmini, kikao cha Jumatano (kesho) ni muhimu sana na ndio kitatupa dira ya mikakati yetu kuelekea msimu ujao wa ligi,” amesema Selemani.

Amesema msimu huu ulioisha hawakufikia malengo waliyojiwekea ikiwamo kurejea tena katika mashindano ya kimataifa kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita ambapo walicheza Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Aidha, Katibu huyo ametoa ufafanuzi juu ya tetesi zinazohusisha klabu hiyo kutaka kumchukua kocha wa zamani wa Kagera Sugar Patrick Odhiambo ili kuifundisha timu hiyo ya mkoani Lindi msimu ujao.

“Tunahitaji kufanya maboresho ya kikosi kulingana na mahitaji ya timu kuhusu suala la kocha hilo ni mapema kulizungumzia kwa sababu bado uongozi hatujakutana, tukikutana na kuweka mikakati yetu ndio tunaweza kuzungumzia masuala yote ya namna gani tutakiimarisha kikosi chetu,” amesema Selemani

Amesema wamenatarajia kufanya maboresho mazuri ya kikosi cha timu yao kwa kufanya usajili wa nyota wenye kiwango bora kwa ajili ya kupambania timu hiyo kurejea katika michuano ya kimataifa mwakani.

Uteuzi: Katibu Mkuu TAMISEMI, Mtendaji Mkuu TANROAD
Wataalam waanza uchunguzi kiikolojia virusi vya Marburg