Mabosi wa Namungo FC wamesema kikosi chao kipo tayari kuanza msimu mpya mwaka 2023/24 baada ya kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya kuwania taji hilo linalosakwa na klabu 16 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.
Namungo FC inayoongozwa na kocha msaidizi wa zamani wa Young Africans, Cedric Kaze, itafungua pazia la Ligi Kuu Bara kesho Jumanne (Agosti 15) kwa kuvaana na Maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko, Ruangwa mkoani Lindi.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chao, Kocha Msaidizi wa Namungo FC, Denis Kitambi, amesema wamekuwa na maandalizi mazuri ambayo yamewasaidia kutengeneza muunganiko, mzuri wa nyota wa zamani.
Kitambi amesema kwa kushirikiana na bosi mpya (Kaze), wameendelea kujiimarisha na wanaamini wako imara kwa ajili ya kupambana kusaka mnatokeo chanya katika kila mechi watakayocheza.
Amesema malengo yao ni kuona timu inafanya vyema kwa kukata tiketi ya kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa mwakani.
“Tumefanya maandalizi mazuri, tumecheza michezo ya kirafiki ambayo imetupa mwanga wa kuona ubora wetu na kuongeza pale penye madhaifu ili tuwe imara, kila kitu muhimu kimefanyika kuelekea mchezo wetu dhidi ya JKT Tanzania,” amesema Kitambi.
Ameongeza wanafahamu ligi itakuwa na ushindani mkubwa kwa sababu kila timu imejiandaa vizuri na kufanya usajili wa kuboresha vikosi vyao.
Amesema wanawaheshimu JKT Tanzania kwa sababu wana uzoefu na hii inatokana na wao kuwahi kucheza Ligi Kuu Bara mnisimu ya nyuma.
“Hatutaichukulia kama timu ndogo kwa sababu walikuwapo muda mrefu kwenye ligi, walishuka na kupanda tena, imefanya usajili mzuri na wana benchi la ufundi imara, tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunabakiza alama tatu nyumbani,” amesema kocha huyo.
Mechi nyingine za Ligi Kuu Tanzania Bara zitakazochezwa kesho Jumanne (Agosti 15) ni kati ya Ihefu dhidi ya Geita Gold wakati Dodoma Jiji itawakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Jamhuri.