Kocha mkuu wa Namungo FC Hemed Suleyman Morocco, amesema hana budi kuwapongeza wachezaji wake kwa kupambana vilivyo dhidi ya Young Africans, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Benjamin Mkapa jana Jumapili (Novemba 22).

Namungo FC waliokua wageni kwenye mchezo huo, walitanguliwa kufungwa dakika ya 13 kupitia kwa kiungo wa Young Africans Carlos Carlinhos, lakini walifanikiwa kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji kutoka Ghana Stephen Sey.

Kocha Morocco ambaye aliiongoza Namungo FC kwa mara ya kwanza baada ya kuajiriwa na uongozi wa klabu hiyo, amesema wachezaji wake walipambana kusaka matokeo uwanjani na walikaribia kufanya hivyo, lakini bahati haikua kwao.

“Ulikua mchezo wenye ushindani mkubwa, haikuwa kazi rahisi wachezaji wangu walipambana kusaka ushindi, tulikaribia kufanya hivyo lakini bahati haikua kwetu.”

“Nimeridhishwa na kiwango cha wachezaji wangu, nitahakikisha tunaendelea kwa kasi hii kwenye michezo yetu mingine ya Ligi Kuu inayofuata,” amesema kocha Morocco aliyechukua nafasi ya Hitimana Thiery ambaye aliachana na Namungo FC mwishoni mwa juma lililopita.

Kwa matokeo hayo Namungo FC imefikisha alama 15 ambazo zinawaweka kwenye nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Young Africans wakifikisha alama 24 wakiwa nafasi ya pili.

Wakati huo huo Namungo FC mwishoni mwa juma hili watakua na mtihani wa kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Rabita FC ya Sudan Kusini.

Hii ni mara ya kwanza kwa Namungo FC kushiriki michuano ya kimataifa, baada ya kumaliza kama mshindi wa pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) kufuatia kufungwa na Simba SC mabao mawili kwa moja mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Pique, Sergi Roberto kuipa mtihani FC Barcelona
Mwanahabari avamia mkutano wa siri