Ushindi wa Sahare All Stars dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa Robo Fainali Kombe La Shirikisho (ASFC), umepokelewa kwa shangwe na viongozi wa Namungo FC.
Sahare All Stars ilitinga hatua ya Nusu Fainali kwa kuichapa Ndanda FC kwa mikwaju ya penati nne kwa tatu, baada ya kumaliza dakka 90 kwa matokeo ya sare ya bao moja kwa moja, huku Namungo FC wakiitandika Alliance FC mabao mawili kwa sifuri.
Uongozi wa Namungo FC umesema unaionea huruma Sahare All Stars kwa ‘kupotea njia’ kutokana na kichapo watakapokutana katika mchezo wa Nusu Fainali utakayofanyika Julai 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini, Tanga.
Afisa Habari wa Namungo FC, Kindamba Namlia, amesema kwa sasa hawaufikirii kabisa mchezo huo na mashabiki wao wanauwaza mchezo wa fainali utakaochezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, Mkoani Rukwa.
“Ni kweli mashabiki wetu watakwenda mjini Tanga kutupa hamasa, lakini wengi zaidi wamesema wao wamejiandaa zaidi kwenda Sumbawanga kwa sababu wanajua kikosi chetu hakiwezi kusumbuliwa na wenyeji wetu,” alisema Namlia.
Kiongozi huyo amesema lengo la Namungo FC msimu huu ni kuona timu hiyo inakata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa na si vinginevyo.
“Tumejipanga kisawasawa, ni kama mtu aliyeamua kufanya kazi ya kuchinja, ina maana akiwa machinjioni kitu kitakacholetewa na mteja basi tunachinja tu, hatuangalii rangi wala saizi, Sahare wamekuja, ni bahati mbaya sana kwao. Tunachofanya kwa sasa ni kuwakatia pasipoti wachezaji wetu ambao hawana kwa ajili ya kusafiri kuelekea mechi za kimataifa,” Amesema Afisa huyo.
Safari ya Namungo kwenye michuano ya Kombe La Shirikisho (ASFC) inayotoa mwakilishi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), ilianza kwa kuichapa Might Elephants bao 1-0, halafu wakawafunga Green Warrios goli 1-0 baadaye wakaiadhibu Biashara United mabao 2-0 na kuifunga Mbeya City mabao 2-1 na kuwachapa Alliance goli 1-0.
Timu hiyo pia imekuwa ikifanya vema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kucheza michezo 16 bila kupoteza, ikishika nafasai ya nne katika msimamo ikiwa na alama 56.