Baada ya kuibana Simba SC na kuiondoa katika mbio za Ubingwa msimu huu 2022/23 kikosi cha Namungo FC kimeapa kuibamiza Azam FC katika mchezo utakaopigwa Juni 13, jijini Dar es salaam.

Jumatano (Mei 03) Namungo FC ikicheza nyumbani Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa mkoani Lindi, iliibana Simba SC kwa kulazimisha sare ya 1-1.

Kocha Mkuu wa Namungo FC, Denis Kitambi, amesema mara baada ya kumalizana na Simba SC aliwapa wachezaji wake mapumziko ya muda mfupi ili kupumzisha miili yao.

“Niliwapa mapumziko ya muda mfupi wachezaji wangu hadi Jumamosi na sasa tunaendelea na maandalizi ya mchezo wetu tutakaoucheza ugenini dhidi ya Azam FC,” amesema Kitambi.

Kocha huyo alisema mapungufu kwenye safu yake ya ushambuliaji ambayo ilikuwa inampasua kichwa kwa sasa yamepungua na safu hiyo inaonekana kuimarika.

Amesema hali za wachezaji kiafya zinaendelea vema na anashukuru hadi sasa hana majeruhi yoyote.

“Hakuna mchezaji ambaye ni majeruhi hadi sasa, na ninashukuru kwa hilo, kikubwa ni kupata matokeo mazuri katika mchezo huo,” ameongeza.

Amesema juma lijalo wanatarajia kuanza safari kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.

Namungo kwa sasa inashikilia nafasi ya 6 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 36 baada ya kushuka dimbani mara 27.

Tanzania, Canada kushirikiana utafiti sekta ya Madini
Mwamnyeto, Morrison waichimba mkwara Marumo