Wakati Young Africans ikiondoka leo Alhamis (Septemba 14) kwenda Rwanda kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan itakayochezwa Jumamosi (Septemba 16), kikosi cha Namungo FC kimewasili jijini Dar kuweka kambi ya juma moja ikiwasubiri mabingwa hao watetezi warejee tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Septemba 20.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Kindamba Namlia amesema awali walitaka kuja Dar es salaam kwa ajili ya kusaka mechi za kirafiki lakini Bodi ya Ligi ikatoa tarehe ya mechi hiyo ambayo awali haikuwekwa kwenye ratiba.
“Tumepata tarehe mpya ya kucheza dhidi ya Young Africans ambayo ni Septemba 20, lakini kwa sababu sisi ni timu ya mpira wa miguu muda wote sisi tuko tayari kucheza, awali tulipanga timu ije Dar es salaam kwa ajili ya mechi za kirafiki lakini kwa bahati nzuri tumeupata mchezo wa ligi tarehe 20,”
“Kwa hiyo hapa ninavyozungumza na wewe timu tayari imeshaingia jijini Dar es salaam tumeweka kambi, tunafanya mazoezi mara mbili, asubuhi gym na jioni mazoezi ya uwanjani, kama tunaweza kupata mechi yoyote ya kirafiki hapa kati kati sawa tutacheza kabla ya mechi yetu dhidi ya Young Africans,” amesema Kindamba.
Aidha, amebainisha kuwa kikosi hicho ambacho kinafundishwa na Kocha Cedrick Kaze kiko vyema na wachezaji wake wote afya zao ziko vizuri na wanaisubiri kwa hamu Young Africans irejee kutoka Rwanda ili wamalizane.
Mpaka sasa Namungo FC haijashinda mechi yoyote ya Ligi Kuu, ikianza kwa kuchapwa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania na mechi ya pili ililazimishwa sare ya bao 1-1 na KMC.