Baada ya kupoteza michezo miwili ya Kombe la Shirikisho, kikosi cha Namungo FC kinaendelea kujifua kuelekea mchezo wa mzunguuko wa tatu wa michuano hiyo hatua ya makundi, ambao utawakutanisha dhidi ya Nkana FC ya Zambia.

Namungo FC ilipoteza mchezo dhidi ya Raja Casablanca kwa kufungwa 1-0 mjini Casablanca, kisha ikapoteza mchezo wa pili dhidi ya Pyramid ya Misri jijini Dar es salaam kwa kufungwa mabao 2-0.

Mchezo wa mzunguuko wa tatu dhidi Nkana FC utachezwa jijini Dar es salaam April 02, ambapo Namungo FC itatakiwa kusaka ushindi wake wa kwanza nyumbani kwenye michuano ya kimataifa hatua ya makundi, ambao utawarejesha kwenye matumaini ya kuwa sehemu ya ushindani katika ‘Kundi D’.

Akizungumzia mchezo huo, Afisa habari wa Namungo Kindamba Namlia amesema: “Kikosi chetu tayari kimeanza mazoezi tangu Jumapili, kwa ajili ya mchezo wetu ujao wa kombe la Shirikisho dhidi ya Nkana ambao tunatarajia kucheza Aprili 2, mwaka huu.

“Bado tunaamini kuwa upo uwezekano wa kufuzu katika hatua ya robo fainali licha ya kutokuwa na matokeo mazuri katika michezo yetu miwili ya kwanza ya hatua ya makundi, lakini hatuangalii yaliyopita bali tunapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika michezo yetu minne iliyosalia,”

Namungo FC mpaka sasa inakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo, ikitanguliwa na Raja Casablanca inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 6 sawa na Pyramid inayoongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku Nkana FC ikiburuza mkia baada ya kufungwa michezo yao miwili kwa idadi kubwa ya mabao kulinganisha na Namungo.

Mwanahamisi aelezea ufundi wa soka la Morocco
Tshishimbi: Tutaifunga Simba kwa Mkapa