Uongozi wa Klabu ya Namungo FC umekanusha taarifa za kuanza mazungumzo na Klabu ya Simba SC, ambayo inatajwa kumuwania Kiungo mshambuliaji wa Tanzania Shiza Ramadhan Kichuya, kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa.

Simba SC imetajwa mara kadhaa kutaka kumrudisha Kichuya kupitia dirisha kubwa la usajili, ambalo litafunguliwa rasmi mwishoni mwa mwezi huu, baada ya kuridhishwa na uwezo wake akiwa Namungo FC.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Namungo FC Omar Kaaya amesema, hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote kati yao na Viongozi wa Simba SC zaidi ya kuona taarifa za Kichuya kwenye mitandao ya kijamii, zikimuhusisha na klabu hiyo Kariakoo-Dar es salaam.

Amesema mbali na mazungumzo na upande wa Simba SC, hata kwa mchezaji husika (Shiza Kichuya) hajasema lolote kama anatamani kuondoka mwishoni mwa msimu huu, huku ikifahamika bado ni mchezaji wao halali kwa mujibu wa mkataba uliopo baina ya pande hizo mbili.

“Bado hakuna taarifa wala mazungumzo yaliyofanyika kati ya Simba SC na Namungo FC juu ya Kichuya, na bado Kichuya hajasema chochote juu ya kuondoka kurudi Simba SC kwani bado mchezaji wetu mbali ya mkataba kufika ukingoni” amesema Kaaya

Kichuya aliondoka Simba SC misimu miwili iliyopita kufuatia changamoto ya kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo, na ndipo alipoibukia Namungo FC, ambako anacheza hadi sasa kwa kiwango cha hali ya juu.

Awali Kichuya alikuwa Simba SC akisajiliwa kutoka Mtibwa Sugar, kabla ya kuuzwa Misri kwenye klabu ya Pharco FC, lakini baadae alirudi Tanzania kutokana na mazingira kuwa magumu katika soka lake.

Simba SC yamkana tena Stephen Aziz Ki
Ugumu wa maisha watajwa ajira za watoto