Uongozi wa Namungo FC umejinasibu kuwa katika mawindo ya Mshambuliaji ambaye ataongeza nguvu kwenye kikosi chao msimu ujao wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Namungo wamejinasibu kuwa katika nafasi hiyo, baada ya kukamilisha usajili wa kiungo kiraka, Erasto Nyoni aliyeachwa na Simba SC, huku wakithibitisha kumnasa Winga ambaye watatantangaza siku chache zijazo.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Zidadu, amesema kwa mujibu wa ripoti ya benchi lao la ufundi hawatokuwa na usajili mkubwa zaidi ya maeneo machache yaliyoainishwa.
Zidadu amesema tayari wameshamsajili mchezaji ambaye anacheza nafasi ya winga, lakini jina lake hawatoliweka hadharani kwa sasa hadi wakamilishe taratibu zote kwa asilimia 100.
“Ripoti ya benchi la ufundi tumeipokea, ipo mikononi mwetu, ilikuwa inaonyesha tuyafanyie kazi maeneo kadhaa lakini ni machache na baadhi tumeshayafanyia kazi, tumemsajili Nyoni na winga mmoja ambaye bado hatujamweka hadharani, muda ukifika tutamtangaza na nafasi iliyobaki kwa sasa ni eneo la Mshambuliaji, mtupiaji mabao ndiyo bado tunamsaka,” amesema mwenyekiti huyo.
Zidadu amesema wanachosaka ni uwezo wa kutupia mabao ya si lazima awe mzawa au wa kigeni, hivyo watamsajili yeyote yule ambaye atawaridhisha na atakuwa na uwezo wanaouhitaji.
“Ripoti haikusema ni mzawa au kutoka nje, kwa hiyo ni matakwa na busara yetu sisi wenyewe itatuongoza tukipata wa ndani ambaye atakuwa mzuri zaidi tutafanya hivyo, ila tukikosa hata nje tutatoka,” amesema Zidadu.
Amesema wanafanya usajili ambao utawarudisha kwenye kwenye kiwango ambacho mashabiki wamekizoea na si hiki cha msimu wa 2022/23, ambao ulimalizika hivi karibuni.
“Ni kweli hatukuwa kwenye kiwango kizuri msimu uliopita, lakini hatutaki kuenda huko sana, tumeshajua tatizo ni nini tumerekebisha baadhi ya mambo na tunaendelea kufanyia kazi mengine ikiwamo usajili bora na panapo majaaliwa tunataka tena nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye mechi za kimataifa.” amesema.
Namungo imemaliza Ligi Kuu msimu huu ikiwa nafasi ya tano ambayo haikutosha kuifanya kucheza michuano yoyote ya kimataifa, pia ikiondolewa mapema kwenye Kombe la ASFC.