Uongozi wa Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi umetoa tamko la kuwa tayari kuialika klabu yoyote ya Ligi Kuu ama Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu ujao wa 2022/23, endapo Klabu ya Namungo FC itarudi katika Uwanja wake wa Majaliwa mjini Ruangwa mkoani humo.
Namungo FC iliutumia Uwanja wa Ilulu kama Uwanja wake wa nyumbani katika msimu wa 2021/22, kufuatia Uwanja wake wa Majaliwa kuwa kwenye matengenezo katika eneo la Kuchezea na Majukwaa.
Meneja wa Uwanja wa Ilulu Halima Kibacha amesema hadi sasa hawana uhakika kama Namungo FC wataendelea kuutumia Uwanja huo kwa msimu ujao, ambao rasmi utaanza katikati ya mwezi Agosti.
Amesema endapo klabu hiyo ya Ligi Kuu itaamua kurudi mjini Ruangwa yalipo maskani yao makuu, watatanga fursa kwa kuzialika klabu nyingine za Ligi Ku una Ligi Daraja la kwanza kuomba kuutumia Uwanja wa Ilulu.
Amesema sharti kubwa ambalo wataipa klabu itakayojitokeza ni kufuata utaratibu ambao utaweka kimkataba, kutokana na mazingira ya Uwanja wa Ilulu kuwa safi na kuvutia katika kipindi hiki.
“Hatuna taarifa zozote kama Namungo FC wataendelea kuutumia Uwanja wetu ama watarudi Ruangwa, tungependa kuona wakiendelea kuutumia Uwanja wetu, lakini ni maamuzi ya Uongozi wao kwa sababu wana Uwanja wao maalum.”
“Ikitokea Namungo FC wanatuthibitishia hawatoutumia Uwanja wetu, tutatangaza fursa kwa klabu za Ligi Kuu ama Ligi Daraja la Kwanza kuutumia Uwanja wa Ilulu kwa msimu ujao, kikubwa watatakiwa kufuata utaratibu tutakaowawekea katika matumizi yao.” Amesema Halima Kibacha
Kabla ya Namungo FC kuutumia Uwanja wa Ilulu msimu wa 2021/22, Uwanja huo ulikua unatumika kwa michezo ya madaraja la chini kwa timu za mkoa wa Lindi pekee.