Katika kukiimarisha kikosi chake, kikosi cha Namungo FC kinatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Singida Fountain Gate itakayofanyika Jumatatu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha imeelezwa.

Akizungumza kutoka Karatu, Kocha Mkuu wa timu hiyo Denis Kitambi, alisema lengo la mchezo huo ni kuangalia uwezo wa kila mchezaji baada ya kuanza maandalizi ya msimu mpya unaotarajiwa kuanza ifikapo Agosti 15, mwaka huu.

Kitambi alisema anaamini mechi hiyo itaanza kumpa mwanga wa kikosi chake wakati bado dirisha la usajili likiwa halijafungwa.

“Tutacheza mchezo wa kirafiki wa kwanza kirafiki Julai 24, mwaka huu na lengo ni kuangalia wachezaji wapya pamoja na wale wa zamani, kwanza tunahitaji kuona mapungufu na ubora wa kila mchezaji,” amesema Kitambi.

Kocha huyo amesema mchezo huo pia utasaidia kuwaweka sawa wachezaji wake ambao wametoka katika mapumziko na kuanza kujiweka tayari kukabiliana na ushindani wa msimu mpya.

“Naweza kusema mpaka sasa tayari tumemaliza kufanya usajili, wachezaji wote wapo kambini hapa Karatu na kwa wale wapya tutawatangaza muda wowote kuanzia sasa. Tutafanya hivyo ili mashabiki wetu wafahamu kinachoendelea ndani ya kikosi chao,” Kitambi amesema.

Ameongeza malengo ya timu yao katika msimu mpya ni kumaliza kwenye nafasi ya juu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wakuliza zao la Vanila waikataa sifuri Kagera
Wayne Rooney ampa baraka Declan Rice