Rais wa Ghana Nana Akufo Addo, ameshinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, kwa kupata asilimia 51.6 ya Kura, dhidi mpinzani wake wa karibu, Rais wa Zamani wa taifa hilo, John Mahama aliyepata asilimia 47.4 ya kura zote.
Rais Akufo Addo ametetea nafasi yake hiyo,dhidi ya mpinzani wake Mahama ambaye tangu awali alionyesha wasiwasi wake wa kutumika kwa nguvu ya Jeshi kwenye uchaguzi huo.
Akiongea muda mfupi baada ya tangazo hilo lililotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya taifa ya Uchaguzi Ghana, Jena Mensa, mjini Accra, Rais Akufo Addo amewashukuru raia kwa kumchagua.
“Nimeguswa tena sana na kuaminiwa nanyi na sichukulii hili kuwa jambo dogo, labda ipo tabia ya kuwa rais aliyepo madarakani akichaguliwa tena muhula wa pili anachukulia hilo kiurahisi na kuanza kupumzika lakini mimi ni wa tofauti, Ninawashukuru sana , Waghana wenzangu kwa ushindi huu” amesema Akufo Addo.
Aidha rais Akufo Addo ameongeza kusema kuwa kazi ya dharura ambayo ataendelea kuifanya ni kuendelea na mchakato wa kugeuza athari ambazo Covid 19 imekuwa nazo katika uchumi na maisha ya kila siku.
Kwa upande wake mpinzani wa Addo, Mahama amelalamikia wizi wa kura.
Awali polisi walisema kulikuwa na kesi 21 wakati wa uchaguzi huo zinazohusiana na ghasia tangu Jumatatu, huku watu watano wakiwa wamefariki
Huu ni uchaguzi wa nane wa Urais tangu Katiba ilivyoandikwa mwaka 1992.