Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amefika Ikulu jijini Dar es Salaam kumpigia goti Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kile alichoeleza kuwa ‘mambo mengi yalitokea hivi karibuni’.

Akizungumza nje ya Ikulu akiwa na Rais Magufuli, Nape ameeleza kuwa aliamua kumuomba msamaha kama Baba na anashukuru kuwa maombi yake yamesikilizwa na amesamehewa.

“Nashukuru amenipa fursa ya kuja kumuona na ameniambia kuwa amenisamehe, na amenipa ushauri. Kwakweli kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru sana, sana,” amesema Nape.

Alieleza kuwa anamshukuru Rais Magufuli pia kwa kumsikiliza na kumuelekeza jinsi ya kuendelea na safari yake ya kisiasa.

Kwa upande wa Rais Magufuli, alieleza kuwa Nape amehangaika sana kutafuta msamaha, ameona dhamira yake na ameamua kumsamehe kwa dhati.

“Nape amekuwa akiomba msamaha, akiandika messages (jumbe) hata usiku wa manane, alikuwa anaomba anione… anione. Hata wasaidizi wangu wamekuwa wakiliona hili,” aliongeza Rais Magufuli akiwa na Nape.

“Amehangaika sana, ameenda hadi kwa Mzee Mangula [Philip Mangula], amefika mpaka kwa Mama Nyerere, amehangaika kweli lakini baadaye… ni katika hiyohiyo kwamba sisi tumeumbwa katika kusamehe. Na leo umemuona asubuhi amekuja hapa, nikaona siwezi kumzuia kuniona, kikubwa anachozungumza ni ‘naomba babu unisamehe,” ameendelea.

“Inauma, kusamehe kunaumiza lakini ninasema kwa dhati kabisa kwamba nimemsamehe,” aliongeza Rais Magufuli.

Katika mazungumzo hayo, Nape alikiri kuwa alikuwa halali na alikuwa hana amani akiutafuta msamaha wa Rais Magufi.

“ulikuwa hauna amani, ulikuwa haulali, ulikuwa hauna amani eeh,” aliuliza Rais Magufuli, na Nape alikiri huku wote wakicheka na kushikana mikono.

Ingawa Nape hakueleza sababu za kuomba msamaha, hivi karibuni kulikuwa na sauti zilizosambaa zilizodaiwa kuwa ni za mazungumzo kati ya Nape na Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Abdulahman Kinana zikiwa na lugha yenye ukakasi kuhusu Rais Magufuli. Sauti nyingine zilizosikika za mazungumzo ya simu zilidaiwa kuwa za Januari Makamba na Baba yake mzee Yusufu.

Septemba 4, 2019, akifungua mkutano wa mwaka wa pamoja wa bodi za wahandisi, Rais Magufuli aliweka wazi kuwa amewasamehe Januari Makamba na William Ngeleja kwakuwa aliwasikia kwenye sauti fulani na kujiridhisha kwa asilimia zaidi ya 100 kuwa ni wao wakimtukana.

Makamba alitumia mtandao wa Twitter kutoa shukurani zake kwa Rais Magufuli kwa kumsamehe.

Kagere, Mayanga waibuka vinara mwezi Agosti
Kodi ya Ardhi kulipwa kwa kutumia simu ya mkononi