Aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kuunda tume huru ya kuchunguza matukio ya uhalifu, utekaji na uvamizi yanayoendelea hapa nchini.
Ameyasema hayo alipokuwa akiongea na wananchi Jimboni kwake Mtama, amesema kuwa kutokana na matukio ya kihalifu yanavyoongezeka kuna haja kubwa ya kuunda tume hiyo huru ili kuweza kuchunguza na kubaini wahusika.
Amesema kuwa haiwezekani vikundi hivyo vya uhalifu vikawa na nguvu zaidi kushinda vyombo vya dola hapa nchini na kusababisha hofu kubwa kwa wananchi.
“Ombi langu kwa Rais Dkt. Magufuli namuomba aunde tume huru ichunguze matendo haya yasijirudie tena kwa sababu yasipochukuliwa hatua yataharibu sura ya Tanzania pia yataweza kuibuka makundi ya wahuni kuanza kuteka watu hovyo,”amesema Nape.
Aidha Mbunge huyo amesema watu wanaofanya mambo hayo wanalengo la kuwagombanisha wananchi na Serikali yao jambo ambalo sio zuri kwa taifa.
Hata hivyo, amesema kuwa mpaka sasa haamini yule mtu aliyemtolea silaha siku ya mkutano wake na waandishi wa habari kama alitumwa na hajui vyombo vya Ulinzi na Usalama vinafanya nini mpaka sasa.