Serikali ya Tanzania haiwezi na haina nia ya kufuta michezo nchini kwa sababu yoyote ile .

Kauli hiyo imetolewa  mjini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye alipokuwa akijibu swali la Mhe. Venance Mwamoto ambaye alitaka kujua kwa nini Serikali isifute Michezo nchini.

Akijibu swali hilo Mhe. Nape alisema kuwa nia ya Serikali ni kuendeleza Sekta ya Michezo kwa maendeleo ya Taifa kwa kuwekeza katika miundombinu ya michezo, Elimu ya Michezo na kushirikiana na wadau wengine na kuhakukisha sekta ya michezo inaendelezwa.

“Naamini kuwa swali lake limelenga kupata maelezo ya kwa nini michezo haiendelei kwa kasi wanayotamani wanamichezo wengi hapa Tanzania na wala siamini kuwa anayo nia ya kutaka Serikali ifute michezo kwa kuwa anafahamu fika umuhimu wa michezo kwa Taifa pamoja na wananchi kwa ujumla”, Alisema Mhe. Nape.

Waziri Nape aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara yake itaendelea kutenga fedha kupitia Bajeti ya Wizara na vyanzo vingine kadri iwezekanavyo ili kuendeleza michezo katika ngazi mbalimbali.

Aidha, alitoa wito kwa wadau wa michezo, ikiwemo Serikali za Mitaa, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, waheshimiwa wabunge, Sekta binafsi na wadau wengine kuibua vipaji vya michezo kwa watoto kuanzia umri mdogo na kuviendeleza.

Akizungumza kuhusu mpango wa Serikali kudhibiti mavazi yasio na staha kwa baadhi ya wasanii nchini, Waziri Nape amesema kuwa Wizara kupitia Baraza la Sanaa la Taifa imekuwa ikitoa elimu kwa wasanii mara kwa mara juu ya umuhimu wa maadili katika sanaa na namna ya kubuni kazi za sanaa zenye ubora unaozingatia maadili ya nchi na jamii.

Pia Waziri Nape ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wasanii nchini wanazingatia nidhamu katika mavazi wanayoyatumia katika kazi zao za sanaa na kuwataka Watanzania kutunza na kulinda maadili na utamaduni wa Mtanzania.

“Ikiwa jamii inayakataa mavazi hayo ili kulinda maadili itapelekea wasanii hao kuona mavazi hayo hayatakiwi, endapo jamii itaonyesha kuyakuwali mavazi hao itapelekea wasanii hao kuona ni kitu cha kawaida na kuzidi kutozingatia maadili,” alifafanua Waziri Nape.

Mavazi ni moja ya utambulisho unaozingatiwa katika Sera ya Taifa ya Utamaduni ya mwaka 1997 inayomtaka Mtanzania ana wajibu wa kulinda mila na desturi sambamba na kuhakikisha maadili yanalindwa na wanawake hawadhalilishwi kupitia kazi za sanaa.

Wakazi wa Magomeni Kota Kunufaika Kwa Miaka Mitano
Mtatiro aukataa uenyekiti wa CUF, Atangaza chama kujiunga na UKUTA