Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye amekinyooshea kidole chama chake hicho akitaka kifumuliwe na kuundwa upya kwani muundo wake ni mzigo.

Nape ameeleza kuwa chama hicho kimejaa idadi kubwa ya watu katika ngazi mbalimbali za uongozi wengi wakiwa hawana tija hivyo kugeuka mzigo wa gharama.

Alisema katika muundo wa Wajumbe wa NEC, hivi sasa kuna wajumbe zaidi ya 400 ambao ni mzigo mkubwa kwa chama ambacho hali yake ya kiuchumi hivi sasa ni ndogo.

“Muundo wetu ni mzigo mzito unaongeza urasimu. Kwa mfano wajumbe wa NEC hivi sasa wapo zaidi ya 400 ni mzigo mkubwa kwa chama matokeo yake walitumia fursa kutafuta ubunge, inahitaji marekebisho makubwa kwa kuwa uchumi wa chama ni mdogo kwa sasa, tunategemea ruzuku tu,” Nape anakaririwa na gazeti la Mwananchi.

Aliongeza kuwa watumishi wa chama wako lukuki lakini kati ya hao ni robo tu ndio wanasiasa hivyo waliobaki wanapaswa kupunguzwa.

Mbunge huyo wa Mtama pia alia na urasimu mkubwa uliopo katika chama hicho kutokana kupitia ngazi nyingi za maamuzi.

“Lazima tupunguze mlolongo wa vikao vya kutoa maamuzi lakini pia tuangalie upya sera na taratibu zetu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Nape alieleza kuwa chama hicho kimejaa majipu ambayo hayanabudi kutumbuliwa ili kukisafisha. Alisema majipu hayo hivi sasa yameficha makucha ndani ya chama.

Kauli hizo za Nape zimekuja ikiwa ni siku chache baada ya CCM kutangaza kuwa itamkabidhi Rais Magufuli Uenyekiti Julai 23 mwaka huu. Zoezi ambalo linaaminika kuwa litafungua mlango wa kuanza kutumbuliwa majipu hayo kama alivyofanya katika ngazi za Serikali.

 

Trump anusurika kifo.
Algeria yapiga marufuku Facebook na Twitter kuzuia wizi wa mitihani