Mbunge wa Jimbo la Mtama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema kuwa kuna haja ya kupitiwa upya kwa sheria inayosimamia thamani ya kura hasa katika kipindi hiki cha wabunge na madiwani kuhama vyama vyao.

Amesema kuwa ni vyema kukawa na sheria ambayo itampa mamlaka mbunge au diwani anayehama chama baada ya uchaguzi, aendelee kuwa na nafasi hizo katika chama anachokwenda ili kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika katika chaguzi ndogo.

Ameyasema hayo akiwa kwenye ofisi ndogo za Bunge visiwani Zanzibar, katika mafunzo ya siku mbili ya kamati ya uongozi, makamu wenyeviti wa kamati za Bunge pamoja na wajumbe wa tume ya utumishi wa Bunge.

Nape amesema kuwa pamoja na uwepo wa wimbi kubwa la wanasiasa kuhama, wapiga kura wanatakiwa kupewa thamani yao kwakuwa wakati wa uchaguzi wao ndio waliowachagua.

“Siwezi kupingana na Katiba kuhusu hamahama za wanasiasa lakini ni vyema thamani ya wapiga kura ikatambulika vyema, bado thamani ya mpiga kura inapaswa kuenziwa,”amesema Nape

Hata hivyo, wakati hayo yakijiri Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally anatarajiwa kufanya  ziara ya kikazi ya siku nne visiwani humo kuanzia leo  Agosti 17 hadi 20 mwaka huu.

 

Chadema yateua watakao gombea, Ukonga,Korogwe na Monduli
Claudio Marchisio aondoka Juventus FC