Siku moja baada ya kusambaa taarifa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye alishikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Singida kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa, mwenyewe amefafanua kilichojili.

Taarifa hizo za uhakika zilieleza kuwa Nape ambaye ni mgombea katika mchakato wa kura za maoni akitafuta nafasi ya kuwakilisha chama hicho kuwania kiti cha ubunge wa jimbo la Mtamba, alikamatwa na maafisa wa Takukuru akiwa maeneo ya Bank ya NMB dakika chache baada ya kuchukua kiasi cha fedha zilizodhaniwa kuwa ni kwa ajili ya kuwahonga wajumbe.

Akifafanua kuhusu tukio hilo na tuhuma zilizomkabili, Nape alikiri kukamatwa na maafisa hao wa Takukuru waliompeleka ofisini kwao kumhoji na baadae kuthibisha kuwa hakuwa na lengo la kuwahonga wajumbe.

“Nadhani hawa jamaa walipotoshwa. Mimi nimekwenda zangu benki kwa lengo la kuchukua fedha, lengo langu ni kuwalipa mawakala wangu. Wakaja hawa jamaa wakajitambulisha kuwa wanatoka Takukuru, wakaniuliza kwa nini ninanichukua fedha nyingi kipindi hiki [cha uchaguzi]? Nikawaambia ‘nakwenda kulipa mawaka, na fedha zenyewe ni milioni 3.6’, Nape aliliambia gazeti la Mwananchi.

Aliongeza kuwa maafisa hao walimchukua hadi ofisini kwao na kumhoji kwa muda usiozidi nusu saa na kujiridhisha kuwa hakuwa na lengo baya kama walivyomdhania awali.

Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Lindi, Stephen Chami alikiri kuwa taasisi hiyo ilijiridhisha baada ya kumhoji Nape, kuwa hakuwa na lengo la kuwahonga wajumbe kama ilivyodhaniwa awali huku akisisitiza kuwa maafisa wake wako macho kila sehemu hivi sasa kwa sababu wanataka kukomesha kabisa vitendo vya rushwa.

Aidha, Nape aliwarushia lawama wapinzani wake kuwa wanafanya kila mbinu kuhakikisha wanamchafua ili asipate nafasi katika uchaguzi wa kura za maoni. Pia, Nape aliwashangaa Takukuru kwa kile alichokiita jicho lao kwa rushwa za masikini na sio zile kubwa zinazotolewa na watu wengine.

“Halafu ninyi [Takukuru], mnaacha marushwa makubwa makubwa huko, watu wanahonga halafu mnamvizia Nape masikini kwa shilingi milioni 3.6?” Nape alinukuliwa.

Leo, CCM inahitimisha zoezi la kuwapata wagombea katika wa nafasi za ubunge kupitia kura za maoni katika sehemu mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam.

 

Dk Slaa: Sipedi Siasa ya Unafiki
Msimamo wa Viongozi CCM Zanzibar Kwa Lowassa Ni Sauti Ya Maelfu Ya Wanachama?