Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amekitaka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumfukuza uanachama aliyekuwa mgombea wake wa urais, Edward Lowassa ili kuunga mkono juhudi za rais John Magufuli kupambana na ufisadi nchini.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Nape alieleza kuwa CCM walimkata Lowassa katika kinyang’anyiro cha kugombea urais kwa sababu ya Ufisadi na kwamba tangu Chadema wamkaribishe katika chama chao, waliachana na ajenda ya kupinga ufisadi.

“Sisi hatukumpitisha [Lowassa] awe mgombea wetu wa urais kwa sababu hiyo ya ufisadi na ndiyo maana yeye mwenyewe aliamua kuondoka na kwenda Chadema. Hata katika kampeni za uchaguzi mkuu, Chadema hawakuzungumzia ajenda ya ufisadi, ni kama Lowassa aliifunika tu,” alisema.

Nape akimsalimia Lowassa, wakati wakiwa wote CCM

Nape akimsalimia Lowassa, wakati wakiwa wote CCM

Nape alionesha kuishangaa kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliyesema kuwa Ufisadi ni ajenda ya kudumu ya chama chao kwa kuwa rais Magufuli hataweza kupambana na ufisadi wote kwa kipindi cha miaka mitano.

Hivi karibuni, Tundu Lissu aliitaka serikali kutoa hadharani majina ya wafanyabiashara wote waliohusika katika sakata la makontena kwa kukwepa kodi kwa kuwa katiba inataja makosa hayo kuwa makosa makubwa ya jinai. Lissu alisema kuwa majina hayo yatasaidia kuwachuja watu wanaotaka uongozi wa serikali.

Alichosema Lowassa kuhusu Viongozi wa Serikali waliomtembelea Sumaye hospitalini
Maalim Seif amwandikia barua Papa Francis kuhusu Zanzibar, Isome hapa