Serikali imesema kuwa Shirika la Habari Nchini (TBC) halitarusha moja kwa moja (live) matangazo ya Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kubana matumizi, na badala yake itarusha vipande muhimu vya mijadala ya Bunge hilo majira ya usiku.

Uamuzi huo wa serikali umebainishwa leo katika kikao cha Bunge hilo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye . Nape amesema kuwa kutakuwa na kipindi maalum cha ‘Leo katika Bunge’ ambacho kitaanza kuanzia majira ya saa nne usiku tofauti na ilivyokuwa awali.

“Kipindi hiki kitakuwa na mambo yote muhimu yaliyojili ndani ya bunge kwa siku husika. Kipindi hiki kitakuwa kinaruka kuanzia saa nne usiku hadi saa tano usiku. Na mheshimiwa Spika kipindi hiki kimeanza kuruka Tarehe 26 Januari 2016, yaani jana na tayari baadhi ya wananchi wameonesha kuridhishwa na utaratibu huu cha kuwa na kipindi maalum usiku,” alisema Nape.

“Uamuzi huu utapunguza gharama za uendeshaji wa Shirika, na pia kupitia kipindi cha leo katika Bunge Watanzania walio wengi watapata nafasi ya kufahamu yaliyojiri Bungeni kwani wakati Bunge linaendelea na mijadala yake Watanzani walio wengi huwa na kazi za kiofisi au nyingine za ujenzi wa Taifa,” aliongeza.

Bado haijawekwa wazi endapo vyombo vya habari vya watu binafsi vitaruhusiwa kurusha moja kwa moja matangazo hayo kutoka Bungeni mjini Dodoma.

Simba Waanika Wazi Msimamo Wao Kuhusu Ratiba Ya VPL
Picha ya kiazi yauzwa kwa zaidi ya shilingi bilioni mbili