Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amezungumzia uwepo wa wimbi kubwa la viongozi wa chama hicho kuhamia katika vyama vinavyounda kambi la Ukawa.

Akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni, Nape alieleza kuwa chama chake kinafahamu wazi kuwa bado kuna baadhi ya viongozi wa chama hicho wataendelea kuhama.

“Tumekuwa tukiulizwa mara nyingi juu ya watu wanaohama kutoka Chama Cha Mapinduzi kwenda vyama vingine na hasa Ukawa. Kwa wale waliohama.. na watakaoendelea kuhama kwa sababu bado wapo wengine tunawasubiri waendelee kwenda,” Nape alisema.

Aliongeza kuwa hakuna kiongozi yoyote wa upinzani aliyeanzisha chama chake bila kutokea CCM. Hivyo, hiyo sio mara ya kwanza kwa viongozi kuondoka katika chama hicho na kuhamia katika upande wa upinzani.

Hata hivyo, Nape alieleza kuwa viongozi wa chama hicho wanaohama wameshindwa kuvumilia na kuheshimu utaratibu wa chama na kulazimisha matakwa yao yatekelezwe kwa maslahi binafsi.

Alimtolea mfano aliyekuwa mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja ambaye alidai alikuwa akisubiriwa kuondoka muda mrefu kumfuata Edward Lowassa ambaye ni rafiki yake. Lakini alichelewa kwa kuwa alitaka kutumia madaraka yake kumpa binti yake nafasi ya ubunge wa viti maalum na kwamba aliposhindwa kufanikisha alitangaza rasmi kuhama chama hicho.

Hata hivyo, Nape alieleza kuwa uzoefu unaonesha kuwa wanaohama Chama Cha Mapinduzi hushindwa kisiasa katika vyama wanavyokwenda.

Katibu Mwenezi wa CCM alipuuza uamuzi wa kuondoka kwa wanachama hao akidai kuwa CCM inawanachama takribani milioni 8, hivyo wanachama wachache wanaoondoka hawawezi kukiadhiri chama hicho.

Picha: Lowassa Apiga ‘Mkwara Mzito’ Mwanza
Baada Ya 3-0, Mourinho Ashabuliwa Mtandaoni