Ngome ya umoja wa upinzani ya Kenya, National Super Alliance (NASA) imedai kuwa kesho itamuapisha Raila Odinga kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya na sio Rais wa Watu kama ilivyokuwa imetangazwa awali.
Afisa Mtendaji Mkuu wa NASA, Norman Magaya amesema mapema leo kuwa kuapishwa huko kwenye utata kutafanyika katika uwanja wa Uhuru Park ambao hutumika kwa matukio makubwa kama hayo, licha ya jeshi la polisi kuonya kuwa hakuna tukio litakalofanyika hapo kesho.
“Tutawaapisha Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kesho kama Rais wa Jamhuri ya Kenya na sio Rais wa Watu. Hatuna nia yoyote ya kubadili uwanja wa kufanyia tukio hilo na kila mbadala ni hapo hapo. Yaani chaguo la kwanza ni Uhuru Park, mbadala ni Uhuru Park,” alisisitiza katika mahojiano aliyofanya na KTN.
Alieleza kuwa wana jaji ambaye anatambulika kisheria ambaye atawaapisha Raila na Kalonzo kwa mujibu wa sheria.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, NASA walifanya mkutano na waandishi wa habari na kuonesha kile walichodai kuwa ni mfumo wa kuhesabia kura unaoonesha namna kura zilivyochakachuliwa na kwamba mshindi alikuwa Raila akimuacha Rais Uhuru Kenyatta kwa zaidi ya kura milioni moja.
- Tafiti: Waendesha bodaboda wanachangia 13% mimba za utotoni
- Darassa azifungukia tuhuma za kutumia dawa za kulevya, ukimya
Walidai Raila alishinda katika majimbo 28 yakiwemo makubwa na Kenyatta alishinda majimbo 21 pekee tofauti na ilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Mahakama ya Juu iliamuru uchaguzi wa Agosti 8 mwaka jana ufutwe kwani haukuwa huru na haki. Mahakama hiyo iliamuru uchaguzi mwingine urudiwe lakini NASA walijiengua kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa marudio uliompa ushindi mnono Rais Uhuru Kenyatta.