Ngome ya upinzani nchini Kenya ya National Super Alliance (NASA) leo imetangaza mabadiliko ya tarehe waliyopanga kumuapisha aliyekuwa mgombea wake wa kiti cha Urais, Raila Odinga kuwa ‘Rais’.

Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Okoa Kenya, kiongozi mwandamizi wa NASA, Musalia Mudavadi amesema kuwa tarehe 12 mwezi huu iliyokuwa inatajwa kuwa siku watakayofanya tukio hilo imeahirishwa hadi watakapotangaza tarehe mpya.

“Kufuatia ushauri tuliopewa na wadau wetu wa ndani na nje ya nchi, uongozi wa NASA unapenda kuwaambia wafuasi wake na umma kwa ujumla kuwa tukio la kumuapisha Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kama Rais na Makamu wa Rais limeahirishwa hadi tutakapowatangazia tena,” alisema.

Aidha, alisema anawaushukuru uongozi wa Mombasa kwa kujitolea eneo la kufanya tukio hilo.

“Tutawatangazia tarehe mpya kwa matukio ya kuapishwa pamoja na uzinduzi wa bunge la wananchi,” Mudavadi anakaririwa.

Odinga alijiondoa kwenye uchaguzi wa marudio ambao ulimpa ushindi wa kishindo Rais Uhuru Kenyatta kisha kuhalalishwa na Mahakama ya juu nchini humo.

Ngome ya NASA imeendelea kusisitiza kuwa haiutambui Urais wa Kenyatta.

Jeshi la Malaysia lajiandaa kuisaidia Palestina ‘kuiokoa’ Jerusalem
Lissu afunguka tena jijini Nairobi