Kambi ya muungano wa vyama vya siasa nchini Kenya inayojulikana kama National Super Alliance (NASA) imesema afya ya mgombea urais wa kambi hiyo, Raila Odinga inaendelea vizuri baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Mwanasiasa huyo ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa taifa hilo alikimbizwa jana katika hospitali ya Mombasa baada ya kusadikika kuwa alikula chakula kisicho salama (food poisoning).
Mshauri wa Odinga, Salim Lone amesema kuwa kiongozi huyo wa upinzani anaendelea vizuri asubuhi hii. Lone aliongeza kuwa NASA itaueleza umma undani wa afya ya mgombea wao.
Odinga alikimbizwa hospitalini jana baada ya hali yake kubadilika alipokuwa katika uwanja wa ndege wa Mombasa akisubiri ndege ya kurejea jijini Nairobi, baada ya kufanya kampeni katika maeneo ya Kilifi.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliongozana na viongozi waandamizi wa muungano huo akiwemo Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula.