Muungano wa vyama vya upinzani vya Kenya unaofahamika kama NASA umetishia kususia uchaguzi mkuu wa nchi hiyo endapo tume ya uchaguzi itapinga uamuzi wa Mahakama uliowaruhusu kuwa na kituo binafsi cha kufanya majumuisho ya kura zao.

NASA imedai kuwa itafanya maandamano makubwa nchi nzima na kususia uchaguzi huo ikiwa tume hiyo itaendelea na mpango wake wa kukata rufaa katika mahakama za juu dhidi ya uamuzi huo.

Umoja huo wa vyama vya upinzani vilivyompitisha waziri mkuu wa zamani, Raila Odinga kuwa mgombea wake wa urais, imekituhumu chama cha Jubilee kuwa kinashirikiana na tume ya taifa ya uchaguzi kufanikisha wizi wa kura.

Hata hivyo, kiongozi wa wabunge wa Jubilee, Adan Duale alisikika ndani ya Bunge la Kenya akiwashutumu NASA kuwa wanapanga njama ya kutumia mfumo wa kielektroniki kuvuruga matokeo ya uchaguzi na kujitangaza kuwa wao ndio washindi.

Katika hatua nyingine, NASA inataka tume iruhusu matokeo ya urais kutangazwa kwenye vituo vya kupigia kura na majimboni, jambo ambalo limepingwa na Tume.

“Vyama vya kisiasa na vyombo vya habari vina Uhuru wa kukusanya matokeo ya chaguzi kwa matumizi yao lakini ni wajibu wa tume ya IEBC kutangaza matokeo hayo,” Mwenyekiti wa tume ya Taifa ya uchaguzi ya Kenya, Wafula Chebukati amekaririwa na Sauti ya Ujerumani.

Mvutano huo unaendelea zikiwa zimebaki takribani siku 84 pekee kufanyika kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa zaidi ya uchaguzi wa mwaka 2013.

Matokeo sita katika mwili wako kama ukila ndizi 2 kila siku
The Game ‘atulia’ na Kendrick kutangaza albam ya mwisho, kuachana na muziki