Msanii wa Hip Hop, Nash MC tayari amewasili nchini Uganda kushiriki katika mradi wa “Muziki wako, Sauti yako” ulioandaliwa na kituo cha utamaduni cha Kijerumani, Goethe Zentrum.
Nash amepata mualiko huo kuwakilisha utamaduni wa Hip Hop nchini baada ya kukidhi vigezo vilivyotakiwa, ambapo watashiriki wasanii kutoka nchi mbali mbali Afrika.
Nchi zilizochaguliwa kuwakilisha sanaa na Hip Hop ni Tanzania, Mauritania, Uganda, Kenya, Rwanda, Senegal na Zimbabwe.
“Napenda kuwajulisha wafuasi wangu na makamanda wangu kuwa leo nimesafiri kuja nchini Uganda katika jiji la Kampala, Namshukuru Mungu kwa kujijalia kufika salama” Amesema Nash baada ya kuwasili nchini Ugana
Aidha, ataiwakilisha Tanzania katika kongamano kubwa linaloitwa “Sanaa na harakati” ambalo litafanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Uganda, ambapo litaongozwa na mwenyeji, Mbunge Bobi Wine.
Pia Nash atashiriki katika onesho kubwa litakalofanyika nchini Uganda, huku wasanii mbali mbali kutoka Afrika, na wasanii kutoka Ujerumani watawakilisha Hip Hop nchini mwao.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Nash MC amesema kuwa wasanii wote waliochaguliwa kutoka nchi za Afrika ni wale wanaowakilisha Hip Hop katika misingi inayokubalika, nyimbo zao ziwe zinalenga jamii yao na kuwatetea watu wa hali ya chini.
Amesema pia wawe na harakati walizoanzisha nchini mwao kwa ajili ya kuielimisha jamii na kujenga katika misingi bora.
“Nashukuru kwa kukidhi vigezo hivyo na kupata nafasi hii ya kuwakilisha katika mradi huu mkubwa wa harakati za sanaa na Hip Hop kwa ujumla” amesema Nash MC.
Video: Lover Boy haukuwa wimbo wa Barnabas, D – Classic afunguka yaliyonyuma ya pazia kuhusu wimbo huo