Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, ameutaka Uongozi wa Klabu hiyo kuendesha mambo yao kwa utaratibu hasa suala la mikataba mpya kwa wachezaji ambao mwishoni mwa msimu huu watamaliza mikataba yao ya sasa.
Rai hiyo kwa viongozi kutoka kwa Kocha Nabi, imekuja kufuatia klabu hiyo kuwa katika mpango mkali wa kuhakikisha wanatimiza lengo la kuwa Mabingwa wa Tanzania msimu huu 2021/22, hivyo wachezaji wanapaswa kufikiria kuipigania timu na sio jambo lingine lolote.
Miongoni mwa wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu ni Saidi Ntibazonkiza, Yassin Mustapha, Bakari Mwamnyeto, Kibwana Shomari, Zawadi Mauya, Farid Mussa, Deus Kaseke na Paul Godfrey.
Chanzo cha Habari kutoka ndani ya klabu ya Young Africans kimeeleza kuwa, Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amekua mkali katika suala hilo, kwa kuwataka viongozi kuwaacha wachezaji wakamilishe majukumu yao, na mambo mengine yafuate baadae.
Chanzo hicho kimeeleza: “Unajua sasa hivi viongozi hawataki kuzungumzia kabisa masuala ya mikataba ya wachezaji ambayo inaisha mwishoni mwa msimu huu.”
“Sababu kubwa ambayo inafanya wao wasizungumzie hilo ni kutaka wabebe ubingwa wa ligi kuu msimu huu na wapo makini sana kwani waliwaambia wachezaji na benchi la ufundi juu ya jambo hilo.”
“Walishakaa kikao na wachezaji ambao wanamaliza mikataba yao na kuwaeleza kila mmoja kwa juhudi zake ndizo zitamfanya kuongezewa mkataba.
“Lakini pia hata wale ambao bado wana mikataba, wameambiwa waendelee kupambana kwani atakayezingua, msimu ujao hatakuwa sehemu ya kikosi.”
“Hivyo suala la wachezaji kuwaza mikataba kwa sasa halipo, wanachofikiria zaidi ni ubingwa wa ligi.”
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 48, baada ya kucheza michezo 18 huku ikiwa klabu pekee ambayo haijapoteza mchezo hadi sasa.