Kiungo Mshambuliaji wa Young Africans Denis Nkane amepewa onyo na Kocha Mkuu wa klabu hiyo Nasreddine Nabi, kufuatia mwenendo wake katika kipindi hiki ambacho anaendelea kuuguza majeraha.
Nkane alisajiliwa Young Africans wakati wa Dirisha Dogo akitokea Biashara United Mara, na mara ya mwisho alionekana akiwa na kikosi cha klabu hiyo kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi Mjini Unguja visiwani Zanzibar.
Kocha Nabi amesema mbali na kiungo huyo kuwa majeruhi kuna shida ameigundua na tayari amekutana naye na kumwambia kwa lengo la kumsaidia katika maisha yake ya soka.
“Napenda kufanya kazi na vijana, unajua vijana wana nguvu, najua anamaumivu lakini bado sijaridhika na mwanzo wake katika timu, alianza vizuri lakini baada ya kufunga kule Zanzibar kuna aina ya maisha ya kuridhika yamemuingia akilini, hii sio nzuri kwake nimemwambia yeye (Nkane) bado ni mchezaji mchanga asidhani ni staa mkubwa.” Amesema Nabi na kuongeza:
“Young Africans imemuamini kuja hapa, anachotakiwa ni kuthibitisha kwamba sisi makocha hatukukosea kumleta hapa, anatakiwa kupigania namba kwa nguvu na sio kuwa wa kawaida tena.”
Nkane bado hajapata nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha Young Africans katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, kutokana na hali yake ya majeraha, lakini anatarajiwa kuonekana baada ya kupona na kuaminiwa na Benchi la Ufundi la klabu hiyo.