Baada ya Kuibamiza Azam FC mabao 2-1, Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi, amesema haikuwa rahisi kupata matokeo hayo kutokana na wenyeji wao (Azam FC) kuwa na wakati mzuri wa kuwakabili wachezaji wake ndani ya dakika 90.
Azam FC ilitangulia kupata bao kupitia kwa Rodgers Kola kabla ya Djuma Shaban kusawazisha kwa Penati na Fiston Mayele kuongeza bao la pili na la ushindi.
Kocha Nabi amesema Azam FC walionyesha kiwango kizuri na alitarajia hilo, hivyo ilimlazimu kusaka mbinu mbadala ambazo zilifanikiwa kuiwezesha timu yake kupata alama tatu katika Uwanja ugenini.
“Azam FC wamecheza vizuri, nilitarajia watacheza hivi na ndio maana nilijaribu mifumo kadhaa ili kufanikisha lengo la ushindi, namshukuru Mungu tumekamilisha mpango huu na tunaondoka na alama tatu, kwenye Uwanja wa ugenini.”
“Kuna wakati baadhi ya wachezjai wangu walicheza tofauti na maelekezo niliyowapa na ndio maana mambo yalikuwa magumu, lakini kwa umakini nilitumia nafasi kama Kocha Mkuu nikasisitiza jambo la kiufundi walinielewa na kurejea katika njia sahihi zilizotupa matokeo haya.” amesema Kocha huyo kutoka nchini Tunisia
Ushindi dhidi ya Azam FC unaiwezesha Young Africans kufikisha alama 51 baada ya kucheza michezo 19, na kuwaacha Mabingwa Watetezi Simba SC iliyocheza michezo 17 kwa alama 11, huku Azam FC wakisalia na alama 28.