Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi, ameanza kupiga hesabu nzito za kuvuna alama sita katika michezo miwili iliyo mbele yake dhidi ya Azam FC na Simba, ambayo anaichukulia kama fainali kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Young Africans bado ipo kileleni kwa kumiliki alama 48, ambazo zinaifanya kuwa na tofauti ya alama 11 dhidi ya Bingwa mtetezi Simba SC iliyocheza michezo 17 na kuambulia alama 37.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema kila mchezo kwake ni sawa na Fainali, lakini michezo hiyo miwili ni migumu zaidi hasa kulingana na ubora wa timu anazokwenda kukutana nazo.
Amesema licha ya kupata matokeo mazuri katika michezo 18 iliyopita, kikosi chake hakiko kwenye ubora ambao unampa jeuri ya kuwabeza wapinzani wao, hivyo wanapaswa kuwaheshimu ili kuhakikisha wanapata alama tatu katika kila mchezo.
“Hii ni michezo migumu kuna Azam FC na Simba SC hasa ukizingatia ni ‘Derby’, ndio kubwa kwa Afrika na huchukuliwa kwa umuhimu hali ambayo kila mmoja anahitaji kupata alama tatu ili kufikia malengo yake,” amesema Nabi.
Amesema anaamini michezo hiyo ni muhimu kuanza kujipanga mapema ili kuhakikisha wanaweka mikakati yao imara, ili kufikia lengo walilojiwekea kama Young Africans.
Mwishoni mwa juma lililopita kikosi cha Young Africans kilicheza dhidi ya KMC FC na kuibuka na ushindi wa 2-0, huku Azam FC ikiichapa Namungo FC mabao 2-1.
Young Africans itaanza kupapatuana na Azam FC mapema mwezi April katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi Jijini Dar es salaam, kisha itacheza dhidi ya Simba SC April 30, Uwanja wa Benjamin Mkapa.