Kocha Mkuu wa Young Africans, Nasreddine Nabi, amesema sasa ni muda wa ‘vita’ mpya wa kusaka alama katika kila mchezo wa Ligi Kuu huku akiwaonya wachezaji wake kutobweteke na nafasi walioko kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Nabi amesema suala la ubingwa amekuwa akiendelea kusisitiza kwa wachezaji wake kuangalia mechi zinazowakabili kwa kuwa makini kutafuta pointi kila mchezo ambao utakuwa mbele yao.
“Mara kwa mara nimekuwa nikizungumza na watu wangu wa benchi la ufundi na wachezaji wangu kuhakikisha tunachukulia mechi zetu ni fainali kwa sababu hili duru la pili kila timu inajipanga kutafuta pointi,” amesema Nabi.
Kuhusu winga Chiko Ushindi kutoonekana uwanjani, Nabi alisema, majeraha ya nyama za paja ndiyo sababu ya kumkosa katika kikosi licha ya kwamba amekuwa akimhitaji.
“Chiko ni usajili nilioupendekeza na nafahamu uwezo wake, amekuwa na majeraha lazima apone kwa asilimia kubwa ili kuja kucheza katika mechi za ushindani,” amesema Nabi.
Young Africans imeendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuichabanga Kagera Sugar mabao 3-0 jana Jumapili (Februari 27), na kufikisha alama 41.