Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Mohammed Nabi ametangazwa kuwa Kocha Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwezi Februari 2022.
Nabi ametajwa kuwa kinara katika nafasi hiyo, kupitia taarifa ya Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’ iliyotolewa mapema leo Jumapili (Machi 06) na kusambazwa katika mitandao ya kijamii.
Kocha Huyo kutoka nchini Tunisia alishindanishwa na makocha wa klabu za Geita Gold FC Fred Felix Minziro na Thiery Hitimana wa KMC FC, na kuibuka kinara kutokana na kuiwezesha timu yake kupata ushindi dhidi ya Kagera Sugar (3-0), Mtibwa Sugar (2-0) na kuambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Mbeya City FC.
Hii ni mara ya pili kwa Kocha Nabi kutwaa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kufanya hivyo mwezi Oktoba 2021, akiunga na Malale Hamsini wa Polisi Tanzania, Salum Mayanga alipokua Tanzania Prisons kwa sasa yuko Mtibwa Sugar, Melis Medo aliyekua Coastal Union na Francis Baraza wa Kagera Sugar.
Katika hatua nyingine Kamati ya Tuzo imemtangaza meneja wa Uwanja wa Azam Complex Sikitu Kilakala kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Februari, kutokana na kufanya vizuri kwenye Menejimenti ya matukio ya Michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu Uwanjani.