Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amesema kikosi chake kitacheza kwa tahadhari kubwa dhidi ya Biashara United Mara, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara Hatua ya 16 Bora.
Young Africans leo Jumanne (Februari 15) itakuwa mwenyeji wa mchezo huo, Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikiwa na lengo la kuvuka hatua ya 16 Bora kuelekea Robo Fainali, halikadhalika kwa wageni wao Biashara United Mara watakua na mpango kama huo.
Kocha Nabi amesema wanakwenda kucheza mpambano wenye ushindani na mtego mkubwa, hivyo ameahidi kuwahimiza wachezaji wake kuwa makini wakati wote.
Amesema tahadhari itakua ngao kubwa kwenye mchezo huo, kutokana na uimara wa kikosi cha Biashara United Mara ambacho kimekua kikiwapa upinzani kila wanapokutana nacho.
“Tutaingia kwa tahadhari kubwa, Biashara United Mara ni timu nzuri ambayo kama tutafanya uzembe tunaweza kupoteza, sitaki hili litokee,”
“Itakuwa mechi ngumu lakini hilo halitaondoa uhalisia wa sisi kupata matokeo mazuri kutokana na namna tulivyojiandaa.” Amesema Kocha huyo kutoka nchini Tunisia.
Young Africans inakutana na Biashara United Mara katika mchezo wa kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa mara ya tatu, baada ya awali kukutana mara mbili na zote vijana wa Jangwani kuwang’oa wapinzani wao.
Kwa mara ya kwanza walikutana katika hatua ya 16 Bora misimu miwili iliyopita na Yanga kupenya kwa penalti baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 90, kisha msimu uliopita zikavaana nusu fainali iliyopigwa mjini Tabora na Yanga kushinda kwa bao 1-0.