Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasredine Mohamed Nabi, amemjibu Kocha Mkuu wa Al Hilal Florent Ibenge, kufuatia kauli yake ya kuwafahamu baadhi ya Wachezaji wa miamba hiyo ya Jangwani.
Young Africans itakua mwenyeji wa Al Hilal kesho Jumamosi (Oktoba 08) katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku mchezo wa Mkondo wa Pili ukitarajiwa kuunguruma mjini Khartoum-Sudan mwishoni mwa juma lijalo.
Kocha Ibenge amekua akitamba kuwafahamu vilivyo baadhi ya Wachezaji wa Young Africans ambao waliwahi kufanya nao kazi akiwa AS Vita ya kwao DR Congo na RS Berkane ya Morocco, hivyo huenda ikawa rahisi kwake kuwapunguza kasi kwa kuweka mbinu za kiufundi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa (Oktoba 07), Kocha Nabi amesema: “Kuhusu Ibenge kuwafahamu wachezaji aliowafundisha hata kama asingewafundisha angewafahamu kupitia TV, kuwafahamu sio shida sababu wachezaji wana mabadiliko makubwa sana toka walipotoka kufundishwa na Ibenge hivyo kuwafahamu wale wachezaji haitasaidia.”
“Hata sisi tunawafahamu baadhi ya wachezaji wao, kwa sababu tulituma watu wetu kwenda kuwaangalia wakati wa mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza dhidi ya St George uliochezwa pale Khatoum-Sudan, pia tulifanya hivyo walipocheza mchezo wa kirafiki wakiwa DR Congo dhidi ya Don Bosco.”
“Japokuwa walikataa michezo hiyo isionyeshwe, lakini Alhamdulullah tuliagiza watu na wakawafatilia na tukapata ripoti zao zote.”
“Kuhusu kikosi ambacho kitacheza kesho, ni mchezo wa kimataifa si vizuri kuweka hadharani itabakia kuwa surprise. Huu mchezo ni mchezo ambao Al Hilal wamejiandaa sana”
Young Africans ilitinga Mzunguuko wa Kwanza kwa matokeo ya jumla 9-0 dhidi ya Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC, huku Al Hilal ikisonga mbele kwa faida ya bao la ugenini, kufutia ushindi wa jumla wa sare ya 2-2.
Ikicheza ugenini Ethiopia dhidi ya St George mwezi Septemba Al Hilal ilikubali kufungwa 2-1, kabla ya kuibuka na ushindi wa 1-0 mjini Khartom.