Beki wa Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City Nathan Ake alikosa sehemu ya mazoezi ya mwisho ya kikosi cha kocha Pep Guardiola kikijiandaa kwa mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Barani Ulaya dhidi ya Real Madrid utakaopigwa baadae leo Jumanne (Mei 09).
Ake ndio kwanza akiwa amerejea baada ya kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, lakini ilibidi kuingia uwanjani akitokea benchi katika kipindi cha pili cha mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Leeds United Jumamosi (Mei 06).
Beki huyo Mholanzi amekuwa tegemeo katika upande wa beki wa kushoto wa Man City tangu kuondoka kwa Joao Cancelo aliyeenda kwa mkopo kwa Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, wakati wa Dirisha Dogo mwezi Januari 2023.
Wachezaji wote wakubwa wa Man City walifanya mazoezi na Guardiola huku kikosi hicho kikijiandaa kulipa kisasi dhidi ya Real Madrid katika Nusu Fainali hiyo ya Ligi ya Mabingwa wa Barani Ulaya.
Nathan Ake
Man City tegemeo lao kubwa liko kwa mshambuliaji wao hatari, Erling Haaland ikiwa ni tofauti kubwa wakati timu hizo zilipokutana miezi 12 iliyopita.
City wanaonekana wakijiandaa kucheza Fainali ya pili mfululizo baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-3 katika mchezo wa mwisho kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu msimu uliopita.
Lakini timu hiyo iliruhusu mabao mawili ndani ya dakika mbili yaliyofungwa na Rodrygo kabla Penati ya Karim Benzema haijakamilisha ushindi katika muda wa nyongeza wakati Real Madrid ikienda kutwaa taji hilo la Ulaya kwa mara ya 14.
Wakati huohuo, timu mbili zenye upinzani mkali nchini Italia, AC Milan na Inter Milan kesho Jumatano (Mei 10) zitacheza mchezo wa mkondo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.