Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert amesema mkosoaji wa rais wa Urusi Vladmir Putin,  Alexei Navalny ambae mpaka hivi sasa hana fahamu na anapatiwa matibabu mjini Berlin, alipewa sumu.

Seibert amesema uchunguzi uliofanyika katika sampuli yake ya damu, kupitia maabara ya kijeshi ya Ujerumani, umeonesha ushahidi usio na mashaka kuwa  Navalny alipewa sumu ya Novichok inayoathiri mishipa ya fahamu.

Wakati huohuo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, amesema kuwa mwanasiasa huyo alinusurika kuuawa na kuongeza kuwa anatarajia Urusi kueleza msimamo wake.

“Hatima ya Alexei Navalny imevutia hisia za ulimwengu wote. Dunia itatafuta majibu kutoka kwa Urusi. Tutawafahamisha washirika wetu wa Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami ya nchi za Magharibi, NATO, kuhusu matokeo haya ya uchunguzi,” amesema Merkel

“Tutashauriana na kuamua hatua mwafaka ya pamoja tutakayochukua kwa kutegemea na kuhusika kwa Urusi. Uhalifu dhidi ya Alexei Navalny ni kinyume na maadili na haki za msingi tunazozilinda,” ameongeza Merkel.

Viongozi kutoka kote ulimwenguni wamelaani tukio la kupewa sumu kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny katika jaribio la kutaka kumuua.

Azam FC: Tunahitaji ubingwa 2020/21
PICHA: Hii kufuru sasa, Young Africans kama Ulaya