Uongozi wa record lebel inayomilikiwa na mwanamuziki Emmanuel Elibarik maarufu Nay wa Mitego, umetoa tamko rasmi la kujitoa kwenye tuzo za muziki Tanzania (TMA) kwa msanii huyo.

Kupitia barua ambayo uongozi huo umeitoa, sababu za kujitoa ni pamoja na kile walichodai kukosa imani na kamati ya usimamizi wa tuzo hizo.

Barua hiyo inasema “Uongozi wa Freenation Rec Label leo tarehe 24/03/2022 inatangaza kujitoa kwenye tuzo za muziki za Tanzania Music Award, hivyo basi msanii Emmanuel Elibarick ‘Nay Wa Mitego’ sio mshiriki wa tuzo hizo uamuzi huu umetokana na uongozi wa Freenation Rec Label Kutokuwa na Imani na Kamati Ya Uchambuzi Wa Kazi ‘Academy’.

Katika barua hiyo uongozi huo umewaomba radhi mashabiki na wadau wa muziki waliopenda kumuona Emmanuel Elibarick ‘Nay Wa Mitego’ Kuendelea kuwepo kwenye hizi tuzo, na kuwataka mashabiki wasitishe kupiga kura kuanzia sasa.

“Uwamuzi huu ni kwaajili ya kutetea haki ya kila msanii na masilahi ya muziki wetu wa Tanzania,” ilisema barua hiyo.

Aidha Uongozi wa Freenation Rec Label umeendelea kuwataka mashabiki na wadau wote kuendelea kumuunga mkono mkurugenzi ‘Ceo’ wa Freenation Rec Label Emmanuel Elibarick ‘Nay Wa Mitego’ kwenye Kazi Yake Ya Mziki.

Nay wa Mitego alichaguliwa kuwania tuzo ya TMA kwenye kipenge cha mwanamuziki bora wa Hip Hop wa kiume.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 25, 2022
Mke wa Mrema aahidi kumrudisha Mrema ujanani