Wadhamini Wakuu wa Ligi Kuu Tanzania Benki ya NBC wamekiri kufurahishwa na mwenendo wa Ligi Kuu msimu huu, baada ya kuingia mkataba wa udhamini na Shirikisho la soka nchini TFF.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC Waziri Barnabas, katika hafla maalum ya kuonyesha Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22, iliyofanyika leo Alhamis (Juni 09), Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Dar es salaam.
Barnabas amesema licha ya kuwa ndani ya mwaka wa kwanza wa udhamini wao, wameona mambo mengi yakiendeshwa kisasa na mwenendo wake unafurahisha, hivyo hawana budi kuzipongeza mamlaka ya soka na wadau wote wa mchezo huo nchini Tanzania.
“Tunashukuru sana kwa hapa tulipofikia, pongezi nyingi ziende ‘TFF’, Bodi ya Ligi ‘TPLB’ pamoja na wadau wengine wa mchezo wa soka nchini Tanzania, kwa namna mambo yanavyokwenda.”
“Sisi tumeingia kwa mwaka wa kwanza katika udhamini, lakini tumefurahi sana kwa yote yanayoendelea katika Ligi Kuu, kwa hiyo nichukuwe nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Azam Media kama washirika wetu katika udhamini, tunashirikiana nao vizuri.”
“Nivishukuru vilabu kwa ushirikiano ambao tunaupata kutoka kwao, tunapata muonekano wa kutosha, waamuzi pia tunawashukuru sana popote walipo kwa kuonesha weledi wao, mashabiki wanaohudhuria katika michezo ya Ligi Kuu pamoja na Waandishi wa Habari kuiongelea vizuri Ligi yetu.”
“Ombi langu moja ni kwamba, sisi kama NBC bado tupo sana katika soka, tunamaliza hii sehemu ya kwanza, lakini bado tuna miaka mingine mbele na tutaendelea kuboresha zaidi udhamini katika zawadi na mambo mengine.” Amesema Barnabas