Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amemsema mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kwa kauli zake za kukosoa uamuzi wa Serikali kuzuia mchanga wa madini uliokuwa ukisafirishwa na kampuni ya Acacia.
Akihutubia katika kijiji cha Zinzirigi mkoani Singida, bila kumtaja jina moja kwa moja, Waziri Nchemba alisema kuwa juhudi za Lissu kutaka kuweka vikwazo kwa uamuzi wa Rais Magufuli baada ya kupokea ripoti mbili za uchunguzi wa makontena ya mchanga zimeishia hewani na kuwataka wazee wa mkoa wa Singida kumuita na kumuasa kuungana na nguvu ya Rais kupambana na unyonyaji.
Alisema kuwa wapo watu ambao walianza kueleza kuwa Serikali ingeingia katika matatizo makubwa endapo itashitakiwa kwa uamuzi wake lakini wamekwama. Alisema hivi sasa wameanza kujificha kwenye kichaka cha kuwanyooshea vidole marais wastaafu ambao wana kinga kwa mujibu wa katiba.
“Na mimi nimpongeze Rais kwa kuuona ule mtego, akaufyatua pyaa! Sasa hivi kama ni gari lao matairi yote, Rais kashayaondoa upepo, yameshalala chini. Maana lile walitaka kutengeneza mtego, yaani ni kama mtu anayepigwa anatafuta mti ili ajifiche,” Nchemba aliwaambia wanakijiji wa Zinzirigi.
“Hawa watu wanatuona kama mazuzu hivi. Rais wetu amechukua hatua tena sio kwa maneno, ni kwa vitendo. Tumuunge mkono,” aliongeza.
Lissu amewahi kukaririwa mara kadhaa akikosoa uamuzi wa kushikilia makontena 277 yenye mchanga wa madini, pia alikosoa matokeo ya ripoti mbili zilizoundwa na Rais Magufuli.
Akijibu kauli za Waziri Nchemba, Lissu amesema kuwa suala la kutowahusisha marais wastaafu ni kwa sababu hawawezekani kwakuwa wana kinga kisheria na sio vinginevyo.
Mbunge huyo ambaye pia ni mwanasheria wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo alieleza kushangazwa na uamuzi wa serikali kukubali kufanya mazungumzo na Acacia na kuachana na suala la kampuni hiyo kufanya biashara nchini kinyume cha sheria, kwa kile kilichodaiwa halijasajiliwa.