Waziri wa Fedha wa Kenya, Prof. Njuguna Ndung’u amesema Serikali ya nchi hiyo haina fedha na hivyo imelazimika kubana matumizi kwa kupunguza baadhi ya shughuli, ikiwamo miradi ya maendeleo na fedha kwa ajili ya mawaziri.
Profesa Ndung’u ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari nchini humo, na kusema Wizara yake imepunguza mgawo wa fedha kwa Mawaziri kwa kiasi cha Shilingi 13.3 bilioni za mawaziri 24 wa Baraza la Rais William Ruto.
Amesema, deni la Taifa limeongezeka na hivyo kuifanya Serikali kuweka nguvu kulilipa deni hilo la Shilingi 8.7 trilioni.
“Bado tuko kwenye shimo, lazima tujue hilo. Hata nyumbani kwako unaweza ukakosa fedha lakini si unanyumba, lakini mahitaji unayotaka ndiyo huwezi kupata yote. Unalinganisha unachoweza kupata na kile ambacho huwezi kupata ndio Serikali inafanya hivyo,” alisema.
Bajeti ya nyongeza ya 2022/2023, mapato ya Serikali ya Kenya kwa Julai hadi Desemba 2022 yalikuwa Sh1.106 trilioni, wakati lengo lilikuwa Sh1.158 trilioni, hivyo kuwa na pungufu la Sh51.8 bilioni.
Pia, kwa mujibu wa bajeti hiyo, Serikali ilipanga kutumia Sh1.448 trilioni, lakini ilitumia Sh1.340 trilioni kutokana na mapato kuwa pungufu ambapo katika bajeti hiyo, magavana walipangiwa mgawo wa Sh425 bilioni, Serikali za Kaunti Sh407 bilioni na Serikali Kuu mapendekezo yalikuwa Sh380 bilioni.
Katika hotuba yake Bungeni, Rais William Ruto alisema ataendelea kupunguza matumizi ya fedha mwaka ujao, kwa kiasi ambacho hakutaja na kuwaambia wabunge kuwa aliiagiza pia Wizara ya Fedha kupunguza matumizi ya Serikali kwa dola za Marekani 2.5 bilioni (sawa KSh. 300 bilioni).
Alisema Serikali inatafuta namna ya kupunguza bajeti ya Taifa ya dola za Marekani 27.4 bilioni hadi kufikia dola 2.5 bilioni kukiwa na punguzo la asilimia 10.
Hata hivyo, Ruto alisema Serikali haistahili kukopa fedha kwa ajili ya kulipa mishahara na gharama nyingine, bali lazima nchi irudi katika nidhamu ya matumizi.
Itakumbukwa Mwaka 2018, Waziri wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich aliwahi kusema Serikali inakabiliwa na matatizo kadhaa katika kufadhili baadhi ya miradi yake ya maendeleo.
Waziri huyo alisema hayo mbele ya kamati ya fedha na bajeti ya Baraza la Seneti kwamba hali hiyo inatokana na mamlaka ya mapato Kenya kushindwa kukusanya kodi kwa kufikia malengo waliopewa katika makadirio ya ukusanyaji wa kodi yaliyopitishwa.
Katika mwaka wa fedha 2018, Sh302 bilioni zilitengwa kwa kaunti za serikali 47 katika uwiano ulio sawa wa mapato yaliyokusanywa, ikimaanisha kuwa katika hali mbaya kiuchumi na mgawanyo huo ungeweza kupungua kufikia Sh285 bilioni.
Kenya inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na mfumko wa bei, deni kubwa na ukame.