Balozi za Magharibi nchini Myanmar zimetoa wito kwa viongozi wa kijeshi nchini humo kujizuia na matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji na raia baada ya vikosi vya usalama vyenye magari ya kivita kupelekwa katika miji kadhaa.
Balozi za Umoja wa Ulaya, Uingereza, Canada na nyingine 11 pia zimelaani kamatakamata ya viongozi wa upinzani na manyanyaso dhidi ya waandishi wa habari na kufungwa kwa mawasiliano baada ya mapinduzi ya Februari Mosi.
Aidha, kwenye taarifa yao wamesema wanaunga mkono madai ya raia wa Myanmar ya demokrasia, uhuru, amani na utulivu na kuongeza kuwa dunia inatazama.
Afisa maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar, Tom Andrews kupitia ukurasa wa twitter ameandika hizi ni dalili za kukata tamaa huku akiwaonya majenerali walioongoza mapinduzi hayo kuwa watawajibishwa kwa hatua zao.